KIPA wa zamani wa Simba, Ahmed Feruz amerejea katika Ligi Kuu Bara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuidakia Namungo akitokea Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship.
Kabla ya kuitumikia Stand United, Feruz alikipiga Kagera Sugar kwa mkopo wa miezi sita akitoka Simba ambako hakuwa anapata nafasi ya kucheza.
Mmoja wa viongozi wa Namungo (hakutaka kutajwa jina) aliliambia Mwanaspoti, klabu hiyo inayonolewa na Juma Mgunda, imemsajili Feruz ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi, hususan eneo la ulinzi.
Mmoja wa watu wa karibu wa Feruz (jina tunalo) amesema kipa huyo ameamua kujiunga na timu hiyo ili aweze kucheza ligi kuu na kuonyesha uwezo wake.
“Namungo ni timu yenye mipango mizuri na ameridhishwa na mazungumzo waliyofanya, anaamini kama atapata nafasi basi anaweza kurudi kwenye kiwango chake.”
Inaelezwa usajili wa kipa huyo ni pendekezo la kocha mkuu, Juma Mgunda ambaye anamfahamu tangu alipokuwa anaifundisha Simba.
Namungo kwa sasa ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 12 kuopitia mechi nane ilizocheza, ikishinda tatu, kutoka sare tatu na kupoteza mbili ikiwa na makipa Jonathan Nahimana, Mussa Malika na Suleiman Said.