MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, amesema maandalizi ya timu hiyo yanaendelea vizuri huku hatua zote muhimu zikifanyika kwa kuzingatia mpango na utaratibu walioujiweka, sambamba na mahitaji ya benchi jipya la ufundi linaloongezwa nguvu chini ya kocha Steve Berker.
Mangungu amesema hadi sasa hakuna jambo linalowapa wasiwasi viongozi wa klabu hiyo, kuwa hali hiyo inaweza kuwa tofauti kwa baadhi ya mashabiki ambao wamekuwa na wasiwasi kutokana na kutokutangazwa rasmi kwa baadhi ya mabadiliko ndani ya timu.
Ameeleza kuwa klabu imeamua kufanyakazi kwa umakini na utulivu, badala ya kutoa taarifa za haraka, ili kuhakikisha kila hatua inayochukuliwa inaleta tija kwa maendeleo ya timu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa Mangungu, benchi la ufundi tayari limetoa maelekezo katika maeneo mbalimbali yanayohitaji maboresho, yote yakilenga kuongeza uwezo na ushindani wa kikosi cha Simba katika mashindano yanayoikabili.
Amesema uongozi unaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kwa umakini mkubwa, na kusisitiza kuwa tathmini ya kina itatolewa mara tu watakapokuwa tayari na mambo yatakapokamilika kikamilifu.
“Yapi maneno mengi yanayosemwa nje ya uwanja ambayo ni propaganda, lakini Simba haitapoteza muda kujibu maneno hayo, bali itaendelea kuthibitisha ubora wake kwa vitendo, si maneno,” Amesema.