Home Habari za michezo SIMBA WAINGIA SOKONI KUSAKA KIMYA MPYA

SIMBA WAINGIA SOKONI KUSAKA KIMYA MPYA

18
0

UONGOZI wa klabu ya Simba umeingia sokoni kutafuta kipa mwingine wa kuziba pengo lililosababishwa na majeraha ya makipa wao Moussa Camara na Yakubu Seleman, hali ambayo imeifanya timu hiyo kubaki na chaguo finyu langoni.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema uwezekano wa Camara kuchelewa kupona pamoja na Yakubu kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja au miwili, umeilazimu klabu kuanza mchakato wa kusaka kipa mbadala.

Ahmed amesema Simba haiwezi kujiweka katika hatari ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mzunguko wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na kipa mmoja pekee, Abel Hussein, anayesaidiwa na makipa wawili kutoka timu ya vijana.

Amefafanua kuwa timu inahitaji kipa mwenye uzoefu mkubwa ili kuhakikisha usalama wa lango na kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kwa mujibu wa ripoti za awali za kitabibu, Camara anaendelea vizuri na anatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa mwezi huu wa Januari.

“Hadi sasa sijapokea taarifa yoyote mpya inayobainisha kama Camara atarejea mwezi huu au kama kutakuwa na mabadiliko yoyote katika matibabu yake,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa kurejea kwa Camara kutachelewa zaidi, basi Simba haina budi kumsajili kipa mwingine ili kuhakikisha timu inakuwa na uhakika na uimara wa kikosi chake kwa mashindano yanayoikabili.

Kuhusu hali ya Yakubu Seleman, Ahmed amesema bado hajapata ripoti kamili kutoka kwa jopo la madaktari, akisisitiza kuwa baada ya kurejea kutoka AFCON watatoa taarifa rasmi kwa mashabiki wa Simba ili kuwaondoa hofu na wasiwasi.