Home Habari za michezo WAGOSI WAPO TAYARI KWA VITA LIGI KUU

WAGOSI WAPO TAYARI KWA VITA LIGI KUU

15
0

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Mohammed Muya amesema wachezaji wa timu hiyo wapo tayari kuendeleza vita na ushindani mechi za Ligi Kuu Bara baada ya kurejea tena huku akitamba keshokutwa Jumamosi watakitonesha kidonda cha Azam FC ilitoka kufungwa katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 mbele ya Yanga waliobeba taji kwa penalti 5-4.

Wagosi wa Kaya waliopo nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu ikicheza mechi nane na kuvuna pointi tisa, watakuwa ugenini kukabiliana na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex, pambano likipangwa kupigwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Muya akisema hawatarajii mechi rahisi kutokana na ushindani uliopo lakini wamejiandaa kupambania pointi tatu ugenini ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.

“Hakuna kinachoshindikana mpira ni mchezo wa makosa dakika 90 zenye mbinu bora na sahihi zitatupa matokeo mazuri ugenini tunaheshimu ubora wa wapinzani wetu na wao wasitarajie mteremko kutoka kwetu,” amesema Muya na kuongeza;

“Tunafahamu imetoka kupoteza taji la Mapinduzi kwa mikwaju ya penati hawatataka kurudia makosa kwa kupoteza pointi tatu Ligi kuu na sisi tumejiandaa kuonyesha ushindani dhidi yao hivyo utakuwa mchezo mzuri na wa ushindani.”

Kocha huyo alisisitiza; “Tutaingia kwa tahadhari na kuwaheshimu wapinzani wetu ni timu ambayo ina historia ngumu kwetu tangu imepanda tukikutana huwa mchezo unakuwa mgumu timu bora ndio inaamua matokeo.”

“Tunatarajia mechi ngumu na ya ushindani tumejiandaa vizuri na tunatarajia matokeo mazuri kwenye mchezo wa huo kutokana na mipango ya benchi la ufundi sambamba na wachezaji wenyewe,” aliongeza.

Rekodi inaonyesha katika mechi ya mwisho uwanjani hapo msimu uliopita timu hizo zilipokutana katika Ligi Kuu, wenyeji Azam ilishinda kwa bao 1-0 na ziliporudiana zilitoka suluhu, lakini katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii 2024, Azam iliifunga Coastal 5-2