Home Habari za michezo MZIKI WA LIGI KUU UMERUDI UPYA KWA KISASI

MZIKI WA LIGI KUU UMERUDI UPYA KWA KISASI

97
0

BAADA ya siku 40 za kupisha Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 na Kombe la Mapinduzi 2026, Ligi Kuu Bara inarejea tena leo kwa mechi moja kupigwa na Dodoma Jiji itaikaribisha Singida Black Stars, kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Mechi hiyo itakayopigwa saa 1:00 usiku, ni ya kisasi kwa Dodoma Jiji kwani kikosi hicho kinachoshika nafasi ya 15 kikiwa na pointi sita, hakijaonja ladha ya ushindi dhidi ya Singida Black Stars Ligi Kuu Bara tangu msimu wa 2024-2025.

Timu hizo mara ya mwisho kukutana ilikuwa pia kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na Dodoma Jiji ilichapwa mabao 2-1, Juni 18, 2025, huku mabao ya Singida yakifungwa na Josaphat Arthur Bada na Jonathan Sowah, ambao hawapo kwa sasa.

Bada anayeichezea JS Kabylie ya Algeria, alifunga bao hilo dakika ya kwanza huku Jonathan Sowah anayecheza Simba msimu huu akifunga la pili kwa penalti dakika ya 7, wakati la Dodoma lilifungwa na Iddi Kipagwile kwa penalti dakika ya 41.

Mechi ya kwanza ya msimu wa 2024-2025, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Liti Singida, Singida ilishinda mabao 2-1, Desemba 12, 2024, yaliyofungwa na Mkenya Elvis Rupia dakika ya 8 na 15, huku la Dodoma likifungwa na Yassin Mgaza dakika ya 58.Dodoma haina mwenendo mzuri katika Ligi Kuu msimu huu, kwani katika mechi nane ilizocheza imeshinda mmoja, ikitoka sare mitatu na kupoteza minne, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa pia mara tisa.Kwa upande wa Singida iliyo nafasi ya 12 na pointi nane, katika mechi tano ilizocheza msimu huu imeshinda mbili, ikitoka sare miwili na kupoteza mmoja na kikosi hicho kimefunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa pia mara nne.Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah, amesema baada ya mapumziko ya muda mrefu kwa sasa kikosi hicho kiko tayari kwa ajili ya kutoa ushindani, licha ya kutambua ugumu anaoenda kukutana nao kutokana na ubora mkubwa wa wapinzani wao msimu huu.Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma, amesema Michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika hivi karibuni visiwani Zanzibar imeongeza morali zaidi, kutokana na aina ya mechi nzuri za kiushindani walizokutana nazo.