Home Habari za michezo WAWILI HATIHATI YANGA

WAWILI HATIHATI YANGA

315
0

KOCHA  Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, anakabiliwa na wakati mgumu baada ya klabu hiyo kutakiwa kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni ili kuendana na kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinazotaka timu kuwa na wachezaji wa kigeni wasiopungua wala kuzidi 12.

Kwa sasa, Yanga ina jumla ya wachezaji 14 wa kigeni, hali inayolazimisha nyota wawili kuondolewa ama kwa mkopo au kuuzwa kabisa ili kutimiza matakwa ya kanuni za ligi. Hatua hiyo imeiweka benchi la ufundi katika kazi kubwa ya kufanya maamuzi sahihi bila kuathiri uimara wa kikosi.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amethibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo akisema uongozi wa klabu tayari unaendelea na mchakato wa kutafuta suluhisho la haraka. Ameeleza kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa umakini mkubwa ili kulinda maslahi ya timu na wachezaji husika.

“Ni kweli tuna wachezaji wa kigeni 14 wakati kanuni zinahitaji 12. Tayari tumeshafanya mazungumzo na klabu mbalimbali kubwa, siyo za hapa Tanzania pekee, kwa ajili ya kuwauza au kuwapeleka kwa mkopo baadhi ya wachezaji wetu,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa ndani ya siku tatu hadi tano zijazo, Yanga itaweka wazi majina ya wachezaji watakaoondoka rasmi, ama kwa mkopo au kwa kuuzwa, mara baada ya makubaliano kukamilika na klabu walizozungumza nazo.

Kwa sasa, Yanga ina nyota wa kigeni akiwemo Djigui Diarra (Mali – Kipa), Frank Assinki (Ghana – Beki), Chadrack Boka (DR Congo – Beki), Kouassi Yao (Ivory Coast – Beki), Moussa Balla Conté (Guinea – Kiungo), Lassine Kouma (Chad – Kiungo),

Mohamed Doumbia (Mali – Kiungo), Duke Abuya (Kenya – Kiungo), Prince Dube (Zimbabwe – Mshambuliaji), Celestine Ecua (DR Congo – Winga), Maxi Nzengeli (DR Congo – Winga), Pacôme Zouzoua, Allan Okello, Mohammed Damaro pamoja na Laurindo Dilson Maria Aurelio.

Hatua zitakazochukuliwa kwa nyota hao wawili zinasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa Yanga, huku wengi wakitarajia maamuzi yatakayoongeza ushindani na uimara wa kikosi kuelekea mechi zijazo.