Home Habari za michezo STEVE BARKER AANZA LIGI KUU KWA SARE

STEVE BARKER AANZA LIGI KUU KWA SARE

1013
0

KOCHA  Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameanza rasmi safari yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa matokeo yasiyoridhisha baada ya timu yake kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa ligi kwa Barker tangu achukue mikoba ya ukocha Desemba 28, mwaka jana.

Simba walionekana kuanza vizuri mchezo huo baada ya kupata bao la mapema dakika ya 19 lililofungwa na mshambuliaji Elie Mpanzu, bao lililowapa Wekundu wa Msimbazi uongozi na kuwapa matumaini ya kupata ushindi katika mchezo huo wa nyumbani.

Hata hivyo, Mtibwa Sugar hawakukata tamaa na waliendelea kupambana hadi kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 60 kupitia Fredrick Maharaj, aliyefunga bao hilo baada ya safu ya ulinzi ya Simba kuonyesha udhaifu.

Mchezo huo ulipigwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ambapo Simba walikuwa wenyeji. Licha ya kuwa na faida ya uwanja wa nyumbani, Simba walishindwa kutumia vyema nafasi walizozipata, hali iliyosababisha wapoteze pointi mbili muhimu.

Katika kipindi cha kwanza, Simba walitawala mchezo kwa kiasi kikubwa na walifanya mashambulizi ya mara kwa mara, lakini safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar ilikuwa imara na kuzuia mabao zaidi licha ya presha kubwa kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi.

Kipindi cha pili kilishuhudia Simba wakiongeza kasi ya mashambulizi, lakini walikosa utulivu mbele ya lango, huku nafasi kadhaa zikipotea.  sare hiyo ilimfanya  Barker kuanza ligi kwa matokeo ya kujifunza huku akitazamiwa kufanya maboresho zaidi kuelekea michezo ijayo.