NYOTA wawili wa kimataifa wa Yanga, Allan Okello na Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’, leo wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC.
Yanga itashuka dimbani ikisaka alama tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha katika msimamo wa ligi, katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Mchezo huo unatajwa kuwa na mvuto wa kipekee kwa mashabiki wa soka, hasa kutokana na uwepo wa nyota wapya waliotua ndani ya kikosi cha Yanga, ambao wanatarajiwa kuonyesha uwezo wao kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki.
Kamwe amesema mashabiki hawatapata tu burudani ya soka safi, bali pia watapata fursa ya kuwaona nyota wapya akiwemo Okello na Depu wakionesha ubora wao ndani ya uwanja.
Ameongeza kuwa uwepo wa wachezaji wapya ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani ndani ya kikosi na kuifanya Yanga iwe imara zaidi katika mbio za ubingwa msimu huu.
“Mbali na hao, pia kuna yule mmoja ambaye tulisema itakuwa saprize. Katika mchezo wa leo, mashabiki wataweza kumuona dhidi ya Mashujaa,” amesema Kamwe, amesisitiza kuwa Yanga ipo tayari kwa ushindi.