MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwataka wasiwe na presha juu ya mustakabali wa mchezaji wao, Morice Abraham, ambaye jina lake limekuwa likitajwa sana katika tetesi za usajili.
Morice Abraham katika siku za hivi karibuni amehusishwa na klabu pinzani Yanga, zikidaiwa kuwa mabingwa hao wanahitaji huduma yake na kumwona kama mchezaji anayefaa kuingia kwenye mipango yao ya baadaye.
Hata hivyo, Ahmed amesema wazi kuwa kwa sasa hakuna uwezekano wa Morice kuondoka Simba kwani bado ana mkataba mrefu unaomlinda mchezaji huyo kuendelea kuitumikia klabu yake ya Msimbazi.
Ahmed amesisitiza kuwa Simba haina hofu yoyote linapokuja suala la wachezaji wenye mikataba ya muda mrefu, akieleza kuwa klabu hiyo ipo salama kisheria na haina shinikizo lolote kutoka kwa timu nyingine.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, hata kama kuna klabu zinazomtamani Morice, hali ya kifedha ya soka la Tanzania haiwezi kuruhusu klabu yoyote kumnunua mchezaji huyo kwa thamani anayostahili, jambo linaloifanya Simba kuwa katika nafasi nzuri zaidi.
“Simba haina hofu na mchezaji mwenye mkataba mrefu. Kwa hapa Tanzania hakuna timu ambayo inaweza kumnunua Morice. Wanaomtamani hawana hela ya kumnunua,” amesema Ahmed.