HATIMAYE sintofahamu imefikia tamati baada ya uongozi wa Klabu ya Simba kukamilisha usajili wa beki wa kati, Ismael Oliver Touré, kutoka klabu ya FC Baniyas ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kujiunga rasmi na wekundu wa Msimbazi.
Simba imemtambulisha rasmi nyota huyo kama mali yao mpya kwa lengo la kuongeza nguvu na uimara katika safu ya ulinzi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuboresha kikosi kinachonolewa na kocha mkuu, Steve Barker.
Touré amejiunga na Simba baada ya kuachana na FC Baniyas hivi karibuni, ambapo alikuwa akishiriki Ligi Kuu ya UAE, hatua inayomfungulia ukurasa mpya katika taaluma yake ya soka barani Afrika.
Beki huyo wa kati anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa soka la ushindani, hali inayotarajiwa kuipa Simba faida kubwa hasa katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa.
Kabla ya kwenda kucheza soka la UAE, Touré aliwahi kuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, timu ambayo wakati huo ilikuwa chini ya kocha Steve Barker.
Uzoefu wa awali kati ya Touré na Barker unatajwa kuwa chachu kubwa ya usajili huo, huku mashabiki wa Simba wakitarajia kuona mchango wake uwanjani akisaidia kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo