Home Habari za michezo TANZANIA YAPANDA NAFASI MBILI UBORA FIFA

TANZANIA YAPANDA NAFASI MBILI UBORA FIFA

141
0

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’imepanda kwa nafasi mbili katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mujibu wa chati ya mwezi Januari 2026 iliyotolewa juzi.

Kutinga hatua ya 16 bora ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizofikia tamati huko Morocco juzi Jumapili, kumeonekana kuibeba Taifa Stars ambayo imepaa kutoka nafasi ya 112 hadi nafasi ya 110 ikiwa na pointi 1186.14.

Katika fainali hizo za AFCON 2026, Taifa Stars ilitoka sare katika mechi mbili na kupoteza michezo miwili, ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.

Wakati Taifa Stars ikipanda, mambo hayajaenda vizuri kwa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo imeporomoka kwa nafasi tatu kutoka ile ya 85 hadi katika nafasi ya 88.

Katika fainali za AFCON 2025, Uganda iliishia katika hatua ya makundi baada ya kuchapwa mechi mbili na kutoka sare moja.

Historia imeandikwa na Morocco ambayo kufanya kwake vizuri katika AFCON 2025 ambapo iliishia fainali, kumeibeba na kuipandisha kwa nafasi tatu.

Morocco sasa ni ya nane katika viwango vya ubora wa dunia na imeweka historia ya kuwa Taifa la kwanza la Kiarabu kuingia katika 10 bora ya viwango vya ubora.

Mabingwa wapya wa AFCON 2025, Senegal wamepanda kwa nafasi saba kutoka nafasi ya 19 hadi katika nafasi ya 12 katika viwango hivyo vya ubora.

Timu iliyopanda kwa nafasi nyingi zaidi ni Cameroon ambayo imepaa kwa nafasi 12, kutoka nafasi ya 57 iliyokuwepo awali hadi katika nafasi ya 45.

Hakujawa na mabadiliko katika nafasi saba za juu ambapo timu zilizokuwepo hapo katika viwango vya mwezi Desemba zimeendelea kusalia katika nafasi zao.

Nafasi ya kwanza inashikiliwa na Hispania, Argentina ni ya pili, Ufaransa iko nafasi ya tatu, ya nne ni England huku Brazil ikiwa ya tano.

Ureno imejichimbia katika nafasi ya sita na nafasi ya saba inaendelea kushikiliwa na Uholanzi.