Home Habari za michezo YANGA KUIFATA AL AHLY MISRI JUMATANO

YANGA KUIFATA AL AHLY MISRI JUMATANO

121
0

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuondoka nchini kesho alfajiri kuelekea nchini Misri, mji wa Alexandria, kwa ajili ya mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly.

Safari hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea pambano gumu la kimataifa linalotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi barani Afrika.

Yanga wanatarajiwa kuikabili Al Ahly ugenini Ijumaa Januari 23 mwaka huu, wakiwa na lengo la kusaka alama tatu muhimu zitakazowaweka katika nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo unatajwa kuwa kipimo kikubwa kwa kikosi cha Yanga katika kampeni zao za msimu huu wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema baada ya mchezo wa jana dhidi ya Mashujaa FC, kikosi kimeanza mara moja maandalizi ya safari hiyo muhimu. Ameeleza kuwa leo timu inafanya mazoezi maalumu ya mwisho kwa lengo la kujiweka sawa kabla ya kuanza safari.

Kamwe amesisitiza kuwa hali ya kikosi ipo vizuri kwani hakuna mchezaji mwenye majeraha, jambo linalompa kocha Pedro Goncalves nafasi ya kuchagua kikosi bora kitakachosafiri kwenda Misri. Ameongeza kuwa ushindani ndani ya timu ni mkubwa huku kila mchezaji akijitahidi kuonyesha ubora wake.

“Timu inatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kuelekea Alexandria. Hakuna majeraha, wachezaji wote wapo vizuri na baada ya mazoezi ya leo, kocha wetu Pedro atachagua wachezaji watakaokuwa kwenye msafara,” amesema Kamwe.