KIKOSI cha wachezaji 24 wa klabu ya Yanga kimeondoka leo kuelekea Cairo, Misri, kwa ajili ya mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya klabu kongwe barani Afrika, Al Ahly, unaotarajiwa kuchezwa Ijumaa.
Mabingwa hao wa Tanzania wanasafiri wakiwa na dhamira ya kuendelea kuandika historia katika michuano hiyo mikubwa ya Afrika, huku benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Pedro Goncalves likiwa na imani kubwa na kikosi kilichochaguliwa kwa pambano hilo gumu.
Katika nafasi ya walinda mlango, Yanga imesafiri na Djigui Diarra, Abuutwalibu Mshery pamoja na Hussein Masalanga
Safu ya ulinzi inaundwa na Bakari Mwamnyeto, Frank Assink, Israel Mwenda, Kibwana Shomari, Yao Kouassi, Ibrahim Bacca, Chadrack Boka na Mohamed Hussein, wakitarajiwa kuhimili mashambulizi ya Al Ahly.
Eneo la kiungo linaongozwa na nyota wenye uzoefu na ubunifu akiwemo Duke Abuya, Allan Okello, Mudathir Yahya, Mohamed Damaro, Maxi Nzengeli, Balla Conte.
Wengine ni Shekhan Ibrahim, Lassine Kouma pamoja na Pacome Zouzoua, ambao wanategemewa kudhibiti mchezo na kuanzisha mashambulizi.
Upande wa ushambuliaji, Yanga imesafiri na Prince Dube, Laurindo Aurélio ‘Depu’ pamoja na Emmanuel Mwanengo, wakitarajiwa kuipa timu hiyo makali ya kusaka mabao muhimu ugenini.
Kwa ujumla, mchezo huo unatajwa kuwa wa presha kubwa kwa pande zote mbili, huku Yanga ikilenga kupata matokeo chanya yatakayoongeza nafasi zake katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.