Home Habari za michezo SIMBA YAPAA TUNISIA, CHAMA NDANI YA KIKOSI

SIMBA YAPAA TUNISIA, CHAMA NDANI YA KIKOSI

274
0

KIKOSI cha wachezaji 22 wa Klabu ya Simba SC kimeondoka alfajiri ya leo kuelekea nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo muhimu wa Kombe la Shirikisho Afrika, unaotarajiwa kuchezwa Januari 24 mwaka huu, katika mwendelezo wa hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Safari hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Simba katika kurejesha matumaini ya kufanya vizuri baada ya mwanzo mgumu, huku benchi la ufundi likifanya maboresho kadhaa kwenye kikosi chake kwa lengo la kuongeza ushindani na ufanisi uwanjani.

Kikosi hicho kimejumuisha mchanganyiko wa wachezaji wapya na wale waliokuwepo awali, akiwemo kiungo Clatous Chama ambaye amerejea rasmi Simba na kutambulishwa usiku wa jana akitokea Singida Black Stars, kisha kuungana moja kwa moja na kikosi kilichosafiri kwenda Tunisia.

Chama, aliyewahi kuitumikia Simba hapo awali kabla ya kujiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja, kisha Singida Black Stars, sasa amerejea tena Msimbazi akitarajiwa kuongeza ubunifu na uzoefu katika eneo la kiungo kuelekea mchezo huo mgumu.

Miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho ni makipa Hussein Abel, Alexander Erasto na Djibrilla Kassali.

Wengine ni Shomari Kapombe, David Kameta, Antony Mligo, Nickson Kibabage, Wilson Nangu, Rushine De Reuck, Ismael Toure, Vedastus Masinde, Yusuph Kagoma.

Naby Camara, Kibu Denis, Elie Mpanzu, Morice Abraham, Neo Maema, Libasse Gueye, Hussein Semfuko, Seleman Mwalimu pamoja na Jonathan Sowah.

Simba ilianza vibaya hatua ya makundi baada ya kupoteza michezo miwili ya awali, hali iliyowavunja moyo mashabiki wake.

Mabadiliko yaliyofanywa ndani ya kikosi na benchi la ufundi yameongeza matumaini mapya ya kupata matokeo chanya, kufufua kampeni ya timu hiyo na kuendelea kupigania nafasi ya kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.