Home Habari za michezo HATUKUJA KUOGOPA BALI KUCHEZA MPIRA, PEDRO

HATUKUJA KUOGOPA BALI KUCHEZA MPIRA, PEDRO

6
0

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani kesho Ijumaa, Januari 23, 2026, kuwakabili wenyeji wao Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Alexandria, nchini humo.

Akizungumza kuelekea mchezo huo mkubwa, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro, amesema wanafahamu ukubwa wa mpinzani wao akieleza Al Ahly ni klabu kubwa zaidi barani Afrika na klabu ya karne, jambo linalowalazimu kuwapa heshima wanayostahili.

Hata hivyo, Pedro amesema heshima hiyo haimaanishi kuwa na hofu, akisisitiza kuwa kama Yanga inataka kuwa sehemu ya historia ya soka la Afrika, haina budi kucheza kwa ujasiri na kuonyesha uwezo wake uwanjani.

“Mwisho wa siku tunakuja kucheza na kujaribu kuwashinda wapinzani wetu, huo ndio mpango wetu wa kesho,” amesema Pedro, akiongeza kuwa michezo mikubwa ndiyo inayojenga timu kufikia viwango vya juu barani Afrika.

Ameeleza kuwa ili kufikia kiwango cha juu, ni lazima kucheza dhidi ya timu bora, akibainisha kuwa ana imani na kikosi chake kwa kuwa kina wachezaji wenye ubora, uzoefu na hamu kubwa ya kupambana kwa ajili ya nembo ya klabu.

Kocha huyo ameongeza kuwa licha ya kundi lao kuwa gumu na lenye timu zenye historia kubwa na mataji mengi Afrika, Yanga ina mipango ya muda mrefu ya kuwa miongoni mwa timu bora barani Afrika.

Ameongeza kuwa baada ya mechi mbili wana pointi nne, hali inayowapa nafasi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi, huku lengo kuu likiwa ni kufuzu kwenda hatua inayofuata.