RAIS Mstaafu wa Awamu ya nne wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amesema viongozi wa Serikali hawatakiwi kuegemea katika klabu moja na kukandamiza nyingine kwa sababu zote ni za Watanzania na wao ni viongozi wa Tanzania.
Kikwete amesema kuwa yeye akiwa Rais aliwahi kuwapa Simba pesa kiasi cha sh milioni 30 kwa ajili ya kununua eneo la Simba.
Kikwete amesema wakati akitoa neno kwenye hafla ya uzinduzi wa harambee ya kuichangia Yanga katika Ukumbi wa Diamond jubilee, jijini Dar es Salaam.
“Kuna wakati Prof. Sarungi na Juma Kapuya walikuwa Mawaziri wa michezo na hawa wote ni Simba kindakindaki lakini hawakutumia nafasi zao kuikandamiza Yanga.
“Nilipokuwa Rais Simba walitaka kununua kiwanja kule Mabwepande lakini hela hawana, Aden Rage alikuja kwangu kuniambia wanahitaji milioni 30 kwa ajili ya Kiwanja nikawaambia hizo mmepata.
“Nayasema haya kwa uwajibu wa Uongozi. kwahiyo Mhe. Waziri Mkuu, Yanga wana shughuli na wewe utoe sikukumbushia kama deni ila nawaombea Wanayanga wenzangu mchango ukamuambie na Mhe. Rais na yeye atoe,” amesema.