MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Libasse Gueye, ameendelea kuthibitisha ubora wake baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC, uliomalizika kwa ushindi wa mabao 2-0 kwa Wekundu wa Msimbazi.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam, Simba ilionyesha uimara na kuendeleza ubabe wake dhidi ya Mashujaa FC, kwa kuondoka na pointi tatu muhimu.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa mapema na Gueye katika dakika ya 27, akitumia vyema nafasi iliyotengenezwa na safu ya ushambuliaji, bao lililowapa Simba morali na udhibiti wa mchezo.
Dakika ya 80, Selemani Mwalimu aliihakikishia Simba ushindi baada ya kufunga bao la pili, lililozima kabisa matumaini ya Mashujaa FC na kuhitimisha mchezo kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0, huku Mashujaa FC wakijaribu kujipanga upya lakini wakishindwa kupenya ngome ya Simba iliyokuwa imara.
Katika kipindi cha pili, Simba iliendelea kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, hali iliyoonesha dhamira yao ya kuondoka na ushindi katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.