KOCHA mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves, amewapa majukumu mazito washambuliaji wake wakiongozwa na Prince Dube na Allan Okello kuhakikisha wanatumia kila nafasi itakayopatikana kuivunja ngome ya Al Ahly katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pedro amesema amefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika safu ya ushambuliaji kwenye mechi ya kwanza, akisisitiza kuwa amewataka washambuliaji wake kuwa makini zaidi katika umaliziaji ili kuipa timu ushindi muhimu nyumbani.
Mbali na Dube na Okello, Laurindo Dilson Maria Aurelio (Depu) pia amepewa jukumu la kuiongoza safu ya ushambuliaji, huku safu ya ulinzi ikiongozwa na nahodha Bakari Mwamnyeto ikipewa kazi ya kuwazuia nyota hatari wa Al Ahly wasiathiri mchezo.
Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaochezwa Jumamosi, Januari 31, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Mchezo huo una uzito mkubwa kwa Yanga katika mbio za kusaka tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali.
Pedro amesema kikosi chake kinahitaji ushindi na kimejipanga kupambana kwa nguvu zote. Ameeleza kuwa kupoteza mechi ya kwanza hakujavunja morali ya wachezaji wake.
“Tulipoteza ugenini, lakini hilo halimaanishi tumeshindwa. Tunahitaji kutumia nafasi tunazopata na kuwa imara katika ulinzi,” amesema Pedro.
Kocha huyo ameongeza kuwa hawaogopi Al Ahly licha ya kuwa timu kubwa barani Afrika, akisisitiza kuwa ili Yanga iwe timu kubwa ni lazima iwashinde wapinzani wakubwa, na tayari wamejipanga kufanya hivyo.
Ikumbukwe kuwa Yanga ilipoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly katika Uwanja wa Borg El Arab jijini Alexandria. Huo ulikuwa mchezo wao wa kwanza kupoteza katika hatua ya makundi msimu huu.
Kwa sasa Yanga ipo nafasi ya pili katika Kundi B ikiwa na pointi nne baada ya michezo mitatu huku Al Ahly wakiongoza kundi hili.