KLABU ya Simba SC imeanza kuonyesha sura ambayo mashabiki wake hawajaiona kwa takribani misimu miwili hadi mitatu iliyopita, hali ambayo uongozi wa klabu hiyo umeeleza kuwa imerejea baada ya kiungo fundi, Clatous Chama, kurudi tena ndani ya kikosi hicho.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia kurejea kwa Chama uwanjani na kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara tangu aliposajiliwa tena akitokea Singida Black Stars, ambapo alionesha kiwango cha juu kilichovutia wengi.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, amesema kurejea kwa Chama kumeleta mabadiliko makubwa ndani ya timu, akisisitiza kuwa kuna vitu ambavyo hawakuviona kwa muda mrefu sasa vimeanza kuonekana tena.
“Hata Chama mwenyewe hapo awali alikuwa hafanyi baadhi ya mambo, lakini baada ya kurejea Simba sasa anaonesha ubora mkubwa ambao ulikuwa umepotea kwa miaka mingi chini ya Mwamba wa Lusaka,” amesema.
Ahmed amesema alifurahishwa na uwezo wa Chama kucheza mechi ya saa 10 :00 jioni, akibainisha kuwa mchezaji huyo alikuwa amezoea mechi za saa 8:00 mchana, jambo lililoonesha kuwa amerejea akiwa na utayari mkubwa wa ushindani.
Kwa mujibu wa Ahmed, ndani ya dakika 90 alizocheza Chama, hakuonekana kupoteza hata nafasi moja, kwani kila mpira alioupata aliutumia kwa usahihi mkubwa, ishara tosha kuwa Simba ya zamani huenda ikawa inarejea tena.