Home Habari za michezo SIMBA TAYARI KWA VITA MKAPA, BARKER

SIMBA TAYARI KWA VITA MKAPA, BARKER

43
0

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema kikosi chake kipo tayari kwa asilimia 100 kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Barker amesema anaamini kucheza mbele ya mashabiki wa Simba ni faida kubwa kwa timu yake, lakini amesisitiza kuwa hilo pekee halitoshi bila wachezaji kujitoa kwa nguvu zote uwanjani ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya dhidi ya mabingwa hao wa Tunisia.

Simba wanashuka dimbani katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Esperance ugenini, hivyo wanahitaji ushindi nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Afrika.

Kocha huyo ameeleza kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kwa mafanikio, huku benchi la ufundi likijikita zaidi katika masuala ya kiufundi, kimbinu na kisaikolojia ili kuhakikisha wachezaji wanaingia uwanjani wakiwa na umakini wa hali ya juu.

“Tunajua tuna faida ya kucheza mbele ya mashabiki wetu, lakini tunapaswa kuwa makini na kujitoa kwa asilimia 100 ili kupata ushindi. Esperance ni timu ngumu na yenye uzoefu mkubwa katika michuano ya Afrika,” amesema Barker.

Ameongeza kuwa anawaamini wachezaji wake na ameridhishwa na kiwango chao katika mazoezi, akisema kila mmoja ameonyesha ari na kiu ya kupambana kwa ajili ya klabu na mashabiki wake

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali na wa ushindani mkubwa, huku Simba ikihitaji matokeo mazuri nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.