Home Habari za michezo YANGA YASHINDWA KUFURUKUTA NYUMBANI SARE

YANGA YASHINDWA KUFURUKUTA NYUMBANI SARE

40
0

YANGA SC imeshindwa kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na mabingwa wa Afrika, Al Ahly, katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Wananchi walianza mchezo kwa kasi na kuonyesha nia ya mapema kutafuta bao, jambo lililowalipa dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza baada ya Ibrahim Bacca kufunga bao la kuongoza akitumia pasi safi kutoka kwa Pacome Zouzoua. Bao hilo liliwapa morali kubwa Yanga na kuwafanya waende mapumzikoni wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha kwanza kilikuwa na ushindani mkubwa, kasi na burudani ya hali ya juu huku vigogo hao wa soka la Afrika wakipambana vikali.

Al Ahly walitengeneza nafasi kadhaa hatari, ikiwemo ile ya Zizo aliyempasia Mahmoud Trezeguet, lakini umakini wa safu ya ulinzi ya Yanga pamoja na kipa uliwanyima mabingwa hao nafasi ya kusawazisha kabla ya mapumziko.

Katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, kipa wa Al Ahly, Shobeir, alionyeshwa kadi ya njano kwa kosa la kuchelewesha mchezo, tukio lililoashiria presha kubwa iliyokuwepo uwanjani na kuongeza joto la pambano hilo.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kuendelea kushambuliana kwa nguvu. Al Ahly waliongeza kasi na kutumia vyema nafasi waliyoipata dakika ya 60, ambapo Aliou Dieng alifunga bao la kusawazisha baada ya kupokea pasi kutoka kwa Trezeguet, na kuufanya mchezo kurejea katika usawa.

Licha ya Yanga kujaribu kusaka bao la ushindi hadi mwisho wa mchezo, ulinzi wa Al Ahly ulisimama imara na kuwalazimisha wenyeji kukubali sare hiyo ya bao 1-1. Kwa upande wa Yanga, kiungo Allan Okello aliendelea kung’ara kwa kutawala eneo la kati kwa utulivu na ubora mkubwa, akithibitisha kuwa ni “star boy” wa kikosi hicho.

Kwa matokeo hayo, Al Ahly wanaendelea kuongoza Kundi B wakiwa na pointi nane, huku Yanga wakishika nafasi ya pili kwa pointi tano. JS Kabylie na AS FAR wanabaki mkiani mwa kundi hilo wakiwa na pointi mbili kila mmoja.