KIUNGO wa Simba SC, Inno Jospin Loemba pamoja na winga Anicet Oura wamekamilisha taratibu zote zinazowaruhusu kucheza mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Baada ya kupata leseni rasmi za mashindano hayo, sasa jukumu linabaki kwa Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, kuamua kama atawatumia nyota hao wapya katika kikosi chake kwenye mchezo huo muhimu wa hatua ya makundi.
Oura na Loemba ni miongoni mwa wachezaji walioungana na Simba katika dirisha dogo la usajili, wakilenga kuongeza nguvu na ushindani ndani ya kikosi hicho katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mchezo wa leo utakuwa wa kwanza kwa klabu hiyo kumtambulisha rasmi Oura kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Oura hajawahi kuonekana kwenye mashindano haya makubwa kwa upande wa ubora, hivyo tunatarajia kumuona endapo kocha Barker atampa nafasi ya kucheza katika mchezo wa leo dhidi ya Esperance,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa matarajio ya Simba ni makubwa kupata ushindi katika mchezo huo wa nyumbani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wao wa kukusanya alama tisa katika michezo mitatu ya hatua ya makundi.
Amesema Simba inaanza kampeni hiyo leo dhidi ya Esperance, kabla ya kuelekea ugenini kukabiliana na Petro de Luanda Februari 6, kisha kurejea nyumbani Februari 13 kuwakabili Stade Malien, zote zikiwa ni mechi muhimu katika mbio za kusaka tiketi ya hatua inayofuata.