LICHA ya matumaini ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuendelea kufifia, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amewataka wachezaji wake kupambana kwa nguvu zote katika michezo iliyosalia ili kulinda heshima ya klabu hiyo kwenye anga la soka la Afrika.
Simba itashuka dimbani Jumamosi Februari 7, 2026, ugenini nchini Angola katika mchezo wa marudiano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda, mechi ambayo Barker anasisitiza ni muhimu kwa hadhi ya klabu.
Barker amesema bado anaamini katika kikosi chake licha ya maumivu ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance ya Tunisia mwishoni mwa wiki iliyopita, akieleza kuwa matokeo hayo hayajavunja morali ya wachezaji wake.
Kocha huyo amebainisha kuwa Simba bado ina nafasi ya kujirekebisha kupitia michezo miwili iliyosalia ya hatua ya makundi, ambayo itaipa timu hiyo fursa ya kusahihisha makosa, kuongeza pointi na kurejesha heshima ya klabu kimataifa.
Ameeleza kuwa mchezo uliopita umekuwa somo muhimu kwa wachezaji wake, hasa katika masuala ya umakini na nidhamu ya mchezo, akisema maeneo hayo yanaendelea kufanyiwa kazi kuelekea mechi zijazo.
“Bado tuna mechi mbili za Ligi ya Mabingwa. Tunapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kupambana kila dakika na kuhakikisha tunaiwakilisha Simba kwa heshima,” amesema Barker, akisisitiza kuwa kila mchezaji anatakiwa kuwajibika ndani ya uwanja.
Simba inahitaji ushindi katika mchezo huo dhidi ya Petro de Luanda ili kujiweka katika nafasi ya kumaliza kundi kwa heshima, ikilenga kufikisha pointi saba katika michezo miwili iliyosalia licha ya ugumu wa kusonga mbele.
Kwa sasa, Wekundu wa Msimbazi wanaendelea kushika mkia wa msimamo wa kundi wakiwa na pointi moja baada ya michezo minne, kinara akiwa ni Stade Malien mwenye pointi nane, akifuatiwa na Esperance ya Tunisia yenye pointi sita na Petro de Luanda mwenye pointi tano.