Home Habari za michezo KAPOMBE APIGA MEZA ANGOLA, TUSAHAU YALIYOPITA

KAPOMBE APIGA MEZA ANGOLA, TUSAHAU YALIYOPITA

0

NAHODHA  wa Simba SC, Shomari Kapombe, ameweka wazi kuwa kipaumbele kikubwa kwa sasa ndani ya kikosi hicho ni kupigania nembo ya klabu katika kila mchezo, hususan kipindi hiki ambacho timu haijawa na matokeo mazuri katika michuano ya kimataifa.

Kapombe amewataka mashabiki wa Simba kusahau matokeo yaliyopita na badala yake kuangalia mbele, amesisitiza umuhimu wa mshikamano na kuongeza nguvu kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Petro de Luanda utakaochezwa nchini Angola.

Amesema kikosi kimeweka akili na nguvu zote kwenye maandalizi ya mchezo huo muhimu, huku wachezaji wakitambua uzito wa pambano hilo kwa heshima ya klabu na matarajio ya mashabiki wao.

Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho kuwakabili wenyeji wao Petro de Luanda katika mchezo utakaopigwa saa 1:00 usiku kwa saa za nchini humo, huku presha kubwa ikiwa juu ya mabega ya kikosi hicho kupata matokeo chanya.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kapombe amesema wachezaji wako tayari kupambana kwa nguvu zote na kuhakikisha wanarejesha heshima ya klabu hiyo kongwe ya Tanzania.

“Malengo yetu ni kupigania heshima ya klabu ya Simba. Tunapaswa kusahau matokeo ya nyuma na kuangalia kilichopo mbele yetu, ambacho ni kusaka pointi tatu dhidi ya Petro de Luanda,” amesema Kapombe.