Home Habari za michezo GUEYE AENDELEE KUTIKISA,PRISONS WAPATE ONYO

GUEYE AENDELEE KUTIKISA,PRISONS WAPATE ONYO

0

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Libass Gueye, ameanza kuonyesha makali yake mapema na kuendelea kuwa tishio kwa safu za ulinzi za timu pinzani, baada ya leo  kuifungia timu hiyo bao lake la pili katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Simba walikuwa ugenini dhidi ya KMC FC na kufanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu kwa ushundi wa mabao 2-0 Wekundu wa Msimbazi walionyesha uthabiti mkubwa na kutumia vyema nafasi walizozipata mbele ya lango.

Seleman Mwalimu aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 37, kabla ya Gueye kuongeza la pili dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza, bao lililowapa utulivu na kuua morali ya wenyeji hao.

Kwa Gueye, hili ni bao lake la pili tangu ajiunge na Simba katika dirisha dogo la usajili. Bao lake la kwanza alilifunga dhidi ya Mashujaa FC dakika ya 75, katika mchezo uliomalizika kwa ushindi wa mabao 2-0. Huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu tangu aliposajiliwa, akionesha mapema kuwa ana kitu cha ziada.

Kasi na uwezo wake wa kumalizia nafasi sasa vinaendelea kuwa kero kwa mabeki wa timu pinzani, ambao wanalazimika kufanya kazi ya ziada kumdhibiti ili asiweze kuleta madhara kama alivyofanya dhidi ya KMC FC na Mashujaa.

Simba wanatarajiwa kushuka tena dimbani Februari 22, 2026, watakapokuwa ugenini dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, huku macho mengi yakielekezwa kwa Gueye kuona kama ataendeleza wimbi lake la mabao.