NYOTA wawili wa Simba SC, Jonathan Sowah na Alassane Kante, wanatarajiwa kurejea kikosini na kuimarisha timu hiyo kuelekea dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC itakayopigwa Machi Mosi, baada ya kukamilisha adhabu ya kukosa mechi tano za michuano ya ndani.
Kwa sasa, mchezo dhidi ya KMC FC unakuwa wa tatu kwa nyota hao kuendelea kuwa nje ya uwanja wakitumikia adhabu waliyopewa kufuatia tukio la mechi dhidi ya Azam FC.
Hadi sasa, Sowah na Kante wamezikosa mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, Mashujaa FC na KMC FC, wakishuhudia wenzao wakipambana kusaka matokeo muhimu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baada ya hapo, watakosa michezo miwili zaidi dhidi ya Greenland FC katika Kombe la Shirikisho la TFF na Tanzania Prisons, kabla ya kurejea rasmi kikosini na kuwa tayari kwa majukumu mazito yanayofuata.
Habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba kuanzia michezo ijayo, ikiwemo dhidi ya Singida Black Stars, TRA FC pamoja na dabi dhidi ya Yanga, nyota hao watakuwa sehemu ya kikosi na kuongeza nguvu katika harakati za kusaka ushindi.
Kurejea kwa Sowah na Kante kunatarajiwa kuongeza ushindani wa namba kikosini, kuimarisha safu ya ushambuliaji na kuipa Simba nguvu mpya kuelekea mechi ngumu na zenye presha kubwa, hususan dabi ya Machi Mosi ambayo mara nyingi huamua mwelekeo wa msimu kwa vigogo hao wa soka nchini.
Katika dabi hiyo, Simba watakuwa ugenini kuwakabili watani wao wa jadi, Yanga, wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mara tano mfululizo mbele ya wapinzani hao, kurejea kwa nyota hao kunatajwa kuwa silaha muhimu ya kusaka heshima na kubadili historia.