Siri Ya Kimya Cha Linah Sanga: Ndege Mnana Aliyesusa Bongofleva?
Kutoka Kileleni Hadi Ukimya Mzito: Nini Kimemsibu Linah ‘Ndege Mnana’ Ndani ya Bongofleva?
Takribani miaka 15 iliyopita, kiwanda cha muziki wa Bongofleva kilishuhudia ujio wa sauti ya kipekee kutoka Tanzania House of Talent (THT)—Linah Sanga, maarufu kama ‘Ndege Mnana’. Akiwa na sauti yenye mamlaka na hisia kali, wengi walimtabiria kufika mbali sana, wakimfananisha na mastaa wa kimataifa kama Celine Dion na Whitney Houston kutokana na malezi yake ya kimuziki kuanzia kanisani.
Hata hivyo, kwa sasa ukweli ni tofauti. Linah amepita zaidi ya miaka miwili bila kuachia wimbo wowote binafsi, hali inayozua maswali mengi: Je, Ndege Mnana amesusa kurekodi?
Enzi za Dhahabu na Ushindi Dhidi ya Diamond Platnumz
Safari ya Linah haikuanza kinyonge. Aliteka hisia za mashabiki kupitia ngoma zake za mapema kama Atatamani (2010), Bora Nikimbie (2010), na Lonely (2011) ambazo zilitamba sana kwenye chati za redio.
Mwangaza wake uling’ara zaidi kwenye Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) mwaka 2011, ambapo alitwaa tuzo ya Msanii Bora Chipukizi kupitia wimbo wake Atatamani (uliotayarishwa na Duke Tachez na Mosse chini ya M Lab). Ushindi huo ulikuwa mkubwa kwani alipokea kijiti hicho kutoka kwa Diamond Platnumz aliyeshinda mwaka 2010, huku akiwabwaga wakali kama Sam wa Ukweli, Sajna, Bob Junior, na Top C.
Uwezo wake ulimfanya aendelee kuwania kipengele cha Msanii Bora wa Kike kwenye TMA kwa mfululizo kuanzia mwaka 2012 hadi 2025.
Ngoma ya Shilingi Milioni 105 na Connection ya Afrika Kusini
Kilele cha mafanikio ya Linah kilionekana mwaka 2014 kupitia wimbo wake Ole Themba, uliotayarishwa na Uhuru nchini Afrika Kusini. Video ya wimbo huo iliyoongozwa na Godfather, inatajwa kugharimu takribani Dola 40,000 (zaidi ya Shilingi milioni 105 za sasa). Inasemekana mdundo wa wimbo huo ulikuwa uwe sehemu ya kolabo ya Davido na Mafikizolo (Tchelete), lakini mambo yalipoingiliana, kila msanii alitoa wimbo wake kivyake.
Hata hivyo, baada ya dhoruba hiyo ya mafanikio, kasi ya Linah ilianza kupungua. Wimbo wake wa mwisho kusikika unaitwa Nyota, uliotoka Desemba 2023 chini ya mtayarishaji Jini x66 (anayetengeneza ngoma za Jay Melody).
Siyo Linah Pekee: Listi ya Akina Dada Waliokaa Kimya
Ukimya wa Linah unamweka kwenye listi moja na wasanii wengine wa kike wa Bongofleva ambao wameamua kuweka maiki chini kwa muda:
-
Queen Darleen: Msanii huyu wa zamani wa WCB Wasafi hajasikika tangu Machi 11, 2020 alipoachia ngoma ya Bachela akimshirikisha Lava Lava.
-
Hamisa Mobetto: Mwanamitindo na mshindi huyo wa Miss XXL After School Bash 2010, sasa ametimiza miaka minne bila kutoa wimbo tangu alipoachia EP yake ya Your Truly (2022).
-
Recho Kizunguzungu: Zao lingine kutoka THT, ana miaka miwili ya ukimya tangu alipoachia wimbo wake wa mwisho Saizi Yangu akimshirikisha Stamina mnamo Julai 2024.
Kufuta Post Instagram: Mbinu Mpya au Kupoteza Hamu?
Kitu kinachoshangaza zaidi ni hatua ya Linah kujiondoa pia kwenye mitandao ya kijamii. Tofauti na wasanii wengi wanaotumia mitandao kupiga promo, Linah amefuta karibu machapisho yote kwenye ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 6.6, na kubakisha picha tatu tu.
Chapisho lake la mwisho lililobaki liliwekwa tangu Mei 9, 2023, likisomeka: “Kila mara naleta mwonekano wa kuvutia na wa kujiamini kwenye Instagram.”
Licha ya ukimya huu, Linah bado anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa sita wa kike wa Bongofleva mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram, akitanguliwa na Hamisa Mobetto, Shilole, Nandy, Vanessa Mdee, na Zuchu. Je, nini kinafuata kwenye hatuzi yake ya muziki? Mashabiki bado wana kiu ya kumsikia tena Ndege Mnana.