Kocha Mngqithi Ndiye Aliyesuka Kikosi Kipya cha Yanga SC! Ali Kamwe Athibitisha
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema kocha mkuu wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi, amekuwa na mchango mkubwa katika mchakato wa usajili wa kikosi kinachojiandaa kwa msimu wa 2026/27 baada ya kufuatilia kwa karibu mwenendo wa timu tangu hatua za mwisho za msimu uliopita.
Kamwe amesema uongozi wa Yanga ulifanya mazungumzo ya kina na Mngqithi, ambaye kwanza alitazama mechi za mwisho za timu na kufanya tathmini ya kikosi kilichokuwepo kabla ya kuwasilisha mapendekezo ya maeneo yaliyohitaji kuongezewa nguvu.
“Tulifanya mazungumzo na kocha kwa muda mrefu. Ameifuatilia timu tangu mechi za mwisho za msimu na kuangalia kikosi ili kubaini wachezaji watakaokuwa sehemu ya mipango yake.
Hivyo ameshiriki kwa asilimia kubwa katika usajili wetu na ameeleza mahitaji yake baada ya kuona timu katika michezo ya mwisho ya msimu,” amesema Kamwe.
Ameeleza kuwa kutokana na ratiba ya maandalizi kubana, klabu imeanza hatua za mwisho za mchakato wa usajili na ipo tayari kuanza kuwatambulisha rasmi wachezaji wapya, huku mashabiki wakitarajiwa kushuhudia sura mpya zitakazoongeza ushindani ndani ya kikosi.
Kamwe amesema lengo la Yanga ni kuhakikisha usajili wote unakamilika kabla ya kuanza rasmi kambi ya maandalizi ya msimu mpya, ili Mngqithi apate muda wa kutosha kufanya kazi na kikosi chake tangu siku ya kwanza.
“Tunaingia kambini Julai 20, 2026. Nina imani ifikapo wakati huo tutakuwa tumemaliza kuwatambulisha wachezaji wetu wote. Baada ya hapo tunaelekea kwenye Siku ya Wananchi, kisha tutajipanga kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Hisani,” amesema Kamwe.