MSHAMBULIAJI wa Simba, Baraka Mwangosi, amesema anachokihitaji sasa ni kuaminiwa na kupewa muda zaidi wa kucheza kutoka kwa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Steve Barker ili aweze kuonesha uwezo wake kamili wa kufumania nyavu.
Mwangosi ameweka bayana kuwa ana kiu kubwa ya mafanikio, hasa baada ya kuanza kuonesha makali yake katika michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, akiahidi kupambana kwa nguvu zote ili kuongeza idadi ya mabao katika mechi zijazo.
Straika huyo alitoa kauli hiyo kufuatia ushindi wa mabao 3-0 walioupata Simba dhidi ya Greenland, ambapo alichangia bao moja lililosaidia timu hiyo kutinga hatua ya 32 bora. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwake tangu ajiunge na wekundu hao katika dirisha dogo la usajili, akitokea Mbeya City.
Licha ya kuanza kwa kishindo, Mwangosi amesema hafurahishwi na bao moja pekee, bali anaangalia mbele zaidi. Ameeleza kuwa ataendelea kufanya kazi kwa bidii mazoezini ili kuimarisha kiwango chake na kuwa msaada mkubwa kwa timu.
“Ninachoangalia ni kufunga mabao zaidi mbele. Sahau bao moja nililofunga, mazuri yanakuja,” amesema Mwangosi na akionesha dhamira ya kuacha alama ndani ya kikosi hicho.
Nyota huyo amesisitiza kuwa hakujiunga na Simba kwa bahati mbaya, bali anaamini katika uwezo wake na yuko tayari kuthibitisha thamani yake kila anapopewa nafasi.
Ameongeza kuwa malengo yao ni kufanya vizuri katika mashindano yote wanayoshiriki msimu huu na kuwapa furaha mashabiki wao.