Home Habari za michezo DERBY BILA MZIZE, GONCALVES ABAKI NA KAZI NZITO

DERBY BILA MZIZE, GONCALVES ABAKI NA KAZI NZITO

0

MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Clement Mzize, hayupo nchini baada ya kusafiri kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi kufuatia kujitonesha tena jeraha lake la goti.

Taarifa zinaeleza kuwa nyota huyo ana uwezekano mkubwa wa kufanyiwa upasuaji baada ya majeraha hayo kujirudia wakati alipokuwa akijiandaa na mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie.

Tukio hilo limezua hofu kwa mashabiki pamoja na benchi la ufundi kuelekea michezo muhimu ijayo.

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya klabu, Mzize hatakuwa sehemu ya mipango ya benchi la ufundi kinachoongozwa na Kocha Pedro Goncalves kuelekea Kariakoo Derby, hali inayotoa pigo kubwa kwa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Daktari wa Yanga, Moses Etutu, amethibitisha kuwa mshambuliaji huyo alipata maumivu ya goti siku moja kabla ya mchezo dhidi ya JS Kabylie uliochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

“Tunakumbuka wote Mzize alipata maumivu ya goti na alipatiwa matibabu hadi kurejea uwanjani, lakini siku moja kabla ya mechi ya JS Kabylie alijitonesha tena. Kwa sasa yupo katika uangalizi maalum,” amesema Etutu.

Ameongeza kuwa licha ya kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari, Mzize hatakuwepo kwenye kikosi kitakachosafiri kwa ajili ya Kariakoo Derby dhidi ya Simba SC.

Kariakoo Derby inatarajiwa kuchezwa Machi Mosi, Uwanja wa New Amaan Complex uliopo visiwani Zanzibar, mechi inayosubiriwa  kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, huku Yanga wakiwa wenyeji wa mchezo huo.