Home Habari za michezo BAADA YA SARE, SIMBA SIMBA YATANGAZA VITA RASMI

BAADA YA SARE, SIMBA SIMBA YATANGAZA VITA RASMI

0

UONGOZI wa Simba umesema sare waliyopata dhidi ya Dodoma Jiji FC imewafanya warudi hatua moja nyuma kimkakati na kufanya tathmini ya kina juu ya makosa yaliyojitokeza, wakiongeza nguvu kuelekea mchezo wao ujao wa Kariakoo Derby dhidi ya Yanga SC.

Simba ililazimishwa sare katika mchezo huo kabla ya kuelekea kwenye pambano kubwa linalotarajiwa kuchezwa Machi Mosi katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Matokeo hayo yamekuwa sehemu ya maandalizi yao kuelekea mechi hiyo yenye presha na ushindani mkubwa.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema sare hiyo ina maana kubwa kwa timu yao kwa kuwa imewaondolea hali ya kujiamini kupita kiasi na badala yake imewaongezea umakini.

“Imeongeza ari na umakini katika mechi ijayo. Tungeshinda, pengine tungejiridhisha kuwa tupo kwenye kiwango cha juu zaidi, lakini matokeo haya yametukumbusha bado tunapaswa kufanya kazi kubwa zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa matokeo hayo hayajashusha morali ya wachezaji, bali yamewapa hamasa mpya ya kupambana kwa nguvu zote katika Derby hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Kwa sasa Simba imerejea Dar es Salaam ikitokea Dodoma na inaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kusafiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya Kariakoo Derby, mechi inayotarajiwa kuamua hatima ya mbio za ubingwa msimu huu.