BAADA ya ushindi mnono dhidi ya JKT Tanzania, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema Kariakoo Derby si mchezo wa kawaida, wachezaji wanapaswa kuwa makini, wenye nidhamu na kupambana kwa dakika zote 90.
Kikosi cha Yanga kimeondoka leo asubuhi kuelekea Visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Kocha huyo amesema maandalizi ya derby yalianza mara tu baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya JKT Tanzania, wakianza kufanya tathmini ya kikosi na kurekebisha makosa madogo yaliyojitokeza.
Pedro amekiri anatambua ukubwa na presha ya derby dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, lakini amesisitiza kuwa kikosi chake kitaingia uwanjani kikiwa na lengo moja tu, kupata ushindi.
Amesema mchezo huo unahitaji maandalizi ya kiakili, umakini wa hali ya juu pamoja na mbinu maalum za kukabiliana na ushindani.
“Tutafanya tathmini ya kikosi chetu ili kuhakikisha tunawatumia wachezaji walio katika ubora na utimamu wa mwili. Mechi kama hii inahitaji maandalizi ya kiakili na mbinu sahihi,” amesema Pedro.
Kocha huyo amepongeza wachezaji wake kwa kuonyesha nidhamu, umakini na kutekeleza maelekezo ya benchi la ufundi katika mchezo uliopita.
Amesema ushindi huo ni matokeo ya maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa wiki nzima, wakilenga kuanza kwa kasi ili kuondoa presha mapema.
Ameongeza kuwa mabao ya mapema yaliwapa wachezaji kujiamini na kuwafanya wamiliki mchezo kwa muda mrefu. amewataka kubaki wanyenyekevu licha ya ushindi huo mkubwa, akisisitiza kuwa bado wana safari ndefu kwenye ligi na kila mechi ina umuhimu wake.
Pedro ameonya kuwa hakuna nafasi ya kuridhika mapema, kwani ushindani ni mkubwa na kila timu inapambana kusaka matokeo chanya.