Home Habari za michezo BAO LA SIMBA LATHIBITIKA HALALI, MWAMUZI MSAIDIZI AFUNGIWA

BAO LA SIMBA LATHIBITIKA HALALI, MWAMUZI MSAIDIZI AFUNGIWA

0

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imetoa adhabu kwa baadhi ya waamuzi kufuatia makosa ya kutafsiri sheria za mpira wa miguu katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku tukio kubwa likiwa ni bao la klabu ya Simba lililokataliwa kwenye dabi dhidi ya Yanga.

Katika taarifa iliyotolewa leo, imeelezwa kuwa mwamuzi msaidizi namba moja wa mchezo huo, Kassim Mpanga kutoka Dar es Salaam, amefungiwa miezi sita baada ya kushindwa kutafsiri kwa usahihi sheria za mchezo katika tukio la dakika ya 70. Katika tukio hilo alikataa bao la Simba akidai kulikuwa na kuotea, lakini baada ya wataalam wa sheria za mpira kufanya tathmini ya video ya tukio hilo, imebainika kuwa hakukuwa na kosa lolote kabla ya bao hilo kufungwa.

Aidha, mwamuzi msaidizi namba mbili wa mchezo huo, Hamdan Said kutoka Mtwara, naye amepewa adhabu ya kufungiwa miezi mitatu kwa kosa kama hilo. Katika dakika ya 61 ya mchezo, aliashiria kuwa mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, alikuwa ameotea na hivyo kusimamisha shambulizi la hatari lililokuwa likielekezwa langoni mwa Simba, lakini tathmini ya wataalam imeonyesha kuwa mchezaji huyo hakuwa katika nafasi ya kuotea wakati mpira ulipopigwa.

Mbali na tukio hilo, mwamuzi huyo pia alishindwa kutafsiri sheria katika mechi nyingine iliyohusisha Namungo na Yanga, baada ya kushindwa kuchukua hatua pale mchezaji Abdulkarim Kiswanya wa Namungo alipovutwa jezi na Mussa Damaro wa Yanga ndani ya eneo la penati. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo lilipaswa kupewa adhabu kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu.

Imeelezwa pia kuwa Desemba 2025 mwamuzi huyo aliwahi kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kutokana na makosa ya aina hiyo, hali inayoonesha kuwa changamoto ya kutafsiri sheria imekuwa ikijirudia.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo pia imemchukulia hatua mwamuzi wa akiba wa mchezo kati ya Simba na Dodoma Jiji, Charles Simon kutoka Dodoma, ambaye amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kuruhusu Dodoma Jiji kufanya mabadiliko ya wachezaji katika mikupuo minne badala ya mitatu kama inavyoelekezwa kwenye Kanuni ya 17:32 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Sambamba na hilo, mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida, ameshushwa daraja la uamuzi kutokana na makosa ya kujirudia ya kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mpira wa miguu.