Home Habari za michezo CHAMOU AENDELEZA REKODI DHIDI YA NAMUNGO

CHAMOU AENDELEZA REKODI DHIDI YA NAMUNGO

0

BEKI wa kati wa TRA United, Chamou Karaboue, ameendeleza rekodi bora katika Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya nyota huyo kufikisha mabao mawili, ambayo yote ameyafunga dhidi ya ‘Wauaji wa Kusini’, Namungo, huku akichezea timu mbili tofauti.

Nyota huyo anayeichezea TRA United kwa mkopo akitokea Simba, alianza kufunga akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi, katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Namungo FC, mechi iliyopigwa, Oktoba 1, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Chamou alifunga bao hilo dakika ya 43, huku mengine yakifungwa na beki, Rushine De Reuck dakika ya 61 na mshambuliaji, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ dakika ya 84.

Baada ya hapo, nyota huyo akajiunga na TRA United kwa mkopo kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari 2026, ambapo aliifungia timu hiyo bao moja likiwa ni la pili kwake msimu huu katika Ligi Kuu, kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo FC, Machi 11, 2026.

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Black Rhino, Arusha, Chamou aliifungia TRA United bao la kwanza dakika ya 62, kwa kichwa safi, akiunganisha mpira wa ‘frii-kiki’, uliopigwa na beki wa kushoto wa zamani wa Simba, Valentin Nouma.

Bao la pili la TRA United lilifungwa na Mganda, Joseph Akandwanaho dakika ya 90+2 baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Namungo, Mussa Malika, aliyekuwa amesogea mbele kidogo ya lango lake.

Chamou aliyezaliwa Novemba 22, 1999, alijiunga na Simba Julai 8, 2024, akitokea Racing Club Abidjan ya kwao Ivory Coast, baada ya kucheza kwa msimu mmoja na nusu, katika dirisha dogo la usajili Januari 2026, akatua kwa mkopo TRA United zamani Tabora United.

Akizungumzia kiwango na uzoefu wa beki huyo, Kocha wa TRA United, Mrundi, Etienne Ndayiragije, alisema usajili wa nyota huyo umeongeza utulivu hasa katika eneo la kujilinda, baada ya kupitia kipindi kigumu cha kukosa balansi maeneo yote.

“Tunafurahia kuona wachezaji wote walioingia dirisha dogo la Januari 2026, wameingia moja kwa moja kikosi cha kwanza na kuonyesha sababu za wao kuwasajili, tulizingatia mahitaji na taratibu tunaanza kuona matunda yake,” alisema Ndayiragije.