KIKOSI cha Yanga kimeanza safari kuelekea Arusha kwa dhamira ya kusaka ushindi katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya TRA United, utakaochezwa Machi 18 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Hatua hiyo inakuja baada ya timu hiyo kukosa pointi tatu katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC, jambo ambalo limeongeza hamasa kwa wachezaji na benchi la ufundi kutafuta ushindi katika mchezo ujao.
Uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi kuwa kikosi hicho kinaenda Arusha kikiwa na lengo la kurekebisha makosa yaliyotokea kwenye mchezo uliopita na kuhakikisha kinapata matokeo chanya.
Yanga inaamini bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri katika ligi iwapo itaendelea kukusanya pointi muhimu katika michezo iliyosalia.
Kwa sasa kikosi hicho tayari kimesafiri kuelekea jijini Arusha ambako kitapambana na wenyeji wao TRA United katika dimba la Sheikh Amri Abeid. Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuhitaji matokeo mazuri.
Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Meneja wa Yanga, Walter Harrison amesema baada ya kumaliza mchezo dhidi ya Azam FC, kikosi kimeendelea na maandalizi ya haraka kuelekea mchezo wao unaofuata dhidi ya TRA United.
Harrison amesema ratiba ya ligi imekuwa ngumu kwa timu nyingi kutokana na wingi wa michezo inayochezwa ndani ya muda mfupi, hali inayowalazimu wachezaji kuwa katika hali nzuri ya kimwili na kiakili ili kuhimili ushindani huo.
“Ratiba imekuwa ngumu tumemalizana na Azam FC, sasa tunaelekea Arusha kusaka pointi tatu muhimu. Baada ya hapo tutasafiri kwenda Dodoma ambako tutacheza na Mtibwa Sugar,” amesema Harrison.
Ameongeza kuwa licha ya ugumu wa ratiba, wachezaji wa Yanga wameendelea kujituma na kupambana ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika kila mchezo, akisisitiza kuwa hakuna mechi rahisi katika hatua hii ya ligi.