OGOPA matapeli, mali haiuzwi , kauli ambayo inaweza kuelezea hatua ya Simba SC baada ya kufanikisha kumbakisha kiungo wao nyota, Elie Mpanzu, ndani ya kikosi hicho.
Hatua hiyo imekuja kufuatia juhudi za Rais wa Heshima wa klabu, Mohammed Dewji, aliyedaiwa kuweka nguvu kubwa kuhakikisha mchezaji huyo haondoki.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Simba SC, Mpanzu amesaini mkataba mpya wa miaka miwili ambao utamuweka ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kwa muda zaidi.
Kabla ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, kulikuwa na tetesi nyingi zikidai kuwa nyota huyo huenda asiongeze mkataba wake, huku zikihusishwa pia na madai ya kuvutiwa na watani wa jadi, Young Africans SC.
Hata hivyo, kusaini kwake kumeweka wazi msimamo wa klabu hiyo katika kulinda rasilimali zake muhimu, huku kikosi hicho kikionyesha dhamira ya kuendelea kuwa imara kuelekea mashindano yajayo.
Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alimpongeza Dewji kwa juhudi zake za kuhakikisha nyota huyo anaendelea kusalia klabuni.
“Pongezi nyingi kwa Rais wetu, Mo Dewji kwa kufanikisha kumbakisha nyota huyu wa kimataifa kutoka DR Congo. Sasa hakuna tena wa kumsumbua kijana wetu,” amesema Ahmed Ally.