NENO kubwa alilowahi kuambiwa kiungo mshambuliaji Abdulaziz Makame na makocha wa Simba na Yanga ni atulize kichwa ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu cha kufika mbali.
Makame aliyezaliwa Aprili 24, 1996, Zanzibar, wakati anafanya mahojiano na Mwanaspoti anasema kipindi anacheza Simba mara nyingi alikuwa anaambiwa na makocha kwamba ni mchezaji mkubwa na kwamba anachopaswa kufanya ni kutuliza akili na atafika mbali, na ilikuwa vivyo hivyo baada ya kujiunga na Yanga 2019/20.
“Kwa asilimia kubwa makocha niliyowahi kupita mikononi mwao nikiwa Simba na Yanga, nilikuwa nikicheza mechi ama nikifanya mazoezi walinikalisha chini na kuniambia tuliza akili yako, zidisha bidii, zingatia nidhamu, kipaji chako ni kikubwa sana utafika mbali,” anasema.
Makame ambaye alijiunga na TRA United Agosti Mosi, 2025, anapoulizwa kama ndoto alizowahi kutabiriwa na makocha wa Simba na Yanga zimetimia? Jibu lake ni jepesi tu, “baadhi yake zimetimia naamini kwa sababu naendelea kucheza zitaendelea kutimia zilizosalia.”ALICHOVUNA KATIKA SOKAMakame hapendi kuweka mafanikio yake hadharani, lakini anakiri mpira wa miguu umemfanyia mambo mengi ya maendeleo ambayo kwa asilimia kubwa ingekuwa nje na hapo huenda asingepata vitu anavyovimiliki:“Siwezi kusema namiliki hiki na kile ama nina miradi hii na ile, lakini nimefanya baadhi ya vitu vya kimaendeleo,” anasema.AMTAJA RWEYEMAMUAnasema wakati anajiunga na Simba, meneja wa klabu hiyo, Patrick Rweyemamu ndiye aliyekiona kipaji chake na alipendekeza asajiliwe kikosi B ambapo alimjenga kujitazama kwa ukubwa katika kazi hiyo.“Nilianza kwa kusajiliwa kikosi B baadaye nikapandishwa timu ya wakubwa kwa mkataba wa miaka minne. Dau la usajili kwa kipindi hicho nilipewa Sh 5 milioni,” anasema Makame na kuongeza:“Ushindani ulikuwa mkubwa hivyo viongozi pamoja na makocha walipendekeza nitolewe kwa mkopo kwa timu za Bara, utoto ulikuwa mwingi na akili yangu nilikuwa nawaza nyumbani zaidi, nikawaomba nirudi Mafunzo, wakaniruhusu.
“Kusema ukweli Rweyemamu ni baba wa wachezaji wengi katika timu mbalimbali za Ligi Kuu na za Championship. maneno hayawezi kutosha kumuelezea namna ambavyo ametusaidia na kutujenga vijana wengi, alituaminisha ni wakubwa wa baadaye na tumekuwa hivyo, hatuna la kumlipa zaidi ya kumuombea kwa Mungu ampe maisha marefu.”Wakati Yanga inamhitaji msimu wa 2019/20 Simba ilirejea tena kuhitaji huduma yake, lakini ikashindikana kujiunga nayo kwa sababu ya kigogo waliyemtumia Jangwani alimaliza kila kitu.“Kwa heshima ya kiongozi aliyenifuata niende Yanga ikabidi nikubaliane naye, lakini kwa asilimia kubwa ningerejea Simba, hivyo siyo kuzidiana dau la usajili kama wengi wanavyodhani,” anasema.Anapoulizwa Yanga ilimpa dau la usajili la kiasi gani, anajibu: “Yanga ilinipa Sh 20 milioni, kusema ukweli klabu hizo mbili kwa maana ya Simba na Yanga zimechangia uchumi wangu kwa kiasi fulani.”USHIKAJI WAKE NA FEI TOTOMakame anasema wamekuwa pamoja na staa wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, zipo tabia za utotoni za kuchekesha ambazo bado anazikumbuka hadi sasa.
“Tukiwa wadogo, ingawa hilo naliamini hadi sasa Fei Toto analifanya, alikuwa anapenda sana kula, mnaweza mkanunua vitu sawa bado atakuomba cha kwako, tulikuwa tunampatia, ukitaka kuamini hilo muulize Adeyun Saleh, naamini hadi sasa anapenda kula ingawa hatujapata muda wa kukaa pamoja kutokana na kila mtu ana majukumu yake,” anasema.Kuhusu kiwango cha Fei Toto anasema ana kipaji ambacho hakielezeki: “Fei amekamilika kila idara, ndiyo maana nashindwa kumuelezea ni mtu wa aina gani, pia nawa-kubali wachezaji wote wa Zanzibar.”Mbali na Fei Toto anamzungumzia Ibrahim Ajibu anayecheza KMC aliyojiunga nayo Agosti 29, 2025 kuwa kati ya vipaji vikubwa alivyowahi kuvishuhudia Tanzania.“Nimecheza na Ajibu tukiwa Simba, jamaa ana kipaji cha juu sana. ujue utofautishe mtu kung’ara na yule mpira wa miguu kuuchezea kajaaliwa na Mwenyezi Mungu, akianza kucheza unaweza ukadhani mpira ni kazi rahisi, hatumii nguvu ndiyo maana alikuwa anaimbwa kila sehemu,” anasema Makame na kuongeza:“Mchezaji mwingine ambaye kipaji chake ni cha juu ni Shaaban Idd Chilunda, ukimwangalia anavyouchezea mpira kuanzia mazoezini unavutiwa kumwangalia, hao ni baadhi tu wapo wengi,” anasema.SIMBA, YANGA ZINA WAKATI MGUMUAnasema kwa namna Ligi Kuu ilivyo ngumu klabu kongwe zinakuwa hazina uhakika wa kupata matokeo kwa timu za daraja la kati:“Tofauti na kipindi cha nyuma Simba na Yanga ilikuwa rahisi kwao kupata matokeo iwe nyumbani ama ugenini lakini siyo kwa sasa, zinapambana sana,” anasema mchezaji huyo.
Anaongeza: “Sisi wenyewe tukijiandaa kucheza nazo tunafanya maandalizi kwa uzito kwani tunajua tunakutana na timu zenye wachezaji wa aina gani, ingawa pia hilo linawapa heshima wachezaji wazawa namna wanavyopambana dhidi ya wageni kuonyesha ushindani wa kiwango cha juu.”
Mbali na hilo anazungumzia namna anavyouona msimu huu, akiamini kwamba ni mgumu na huenda bingwa asijulikane mapema. “Ni msimu mgumu, inaweza ikatokea hadi dakika za mwisho asijulikane bingwa mapema na zipi zinazotakiwa kucheza playoff (mtoano) ama kushuka daraja, hilo linatusaidia wachezaji kulinda viwango vyetu,” anasema.






