Home Habari za michezo YANGA YAPUMUA DUBE, BOKA, BACCA WARUDI VITANI

YANGA YAPUMUA DUBE, BOKA, BACCA WARUDI VITANI

0

NYOTA wa Yanga SC, Prince Dube, Chadrack Boka pamoja na beki Ibrahim Abdullah maarufu kama Bacca, wamerejea uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakiwasumbua.

Wachezaji hao walikosa michezo kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na majeraha, lakini sasa wako katika hali nzuri kiafya na wanatarajiwa kujiunga rasmi na kikosi kitakachoingia kambini Machi 31, 2026 kwa ajili ya maandalizi ya mechi zijazo.

Akizungumza kuhusu hali ya kikosi hicho, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kurejea kwa nyota hao ni habari njema kwa timu, huku akibainisha kuwa wachezaji wote kwa sasa wako fiti na tayari kwa majukumu yaliyo mbele yao.

“Wachezaji wote wako katika hali nzuri, na wale waliokuwa majeruhi akiwemo Dube, Boka na Bacca, wanatarajiwa kuingia kambini Jumanne, Machi 31 kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu,” amesema Kamwe.

Hata hivyo, Kamwe ameeleza kuwa kiungo Laurindo Dilson Maria Aurélio maarufu kama Depu bado anaendelea na uangalizi wa madaktari, akitarajiwa kurejea mazoezini baada ya wiki moja.

Ameongeza kuwa kikosi hicho kitaingia kambini Jumanne kuendelea na maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika mchezo huo, Yanga watakuwa nyumbani Aprili 4, 2026, wakiiwakaribisha Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.