MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, ameendelea kuwachokoza wapinzani wao wakubwa akiwemo Simba, kwa kueleza kuwa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara hawatatoa nafasi ya kupoteza hata alama moja.
Kauli hiyo ya Kamwe imekuja kufuatia ujio wa kocha msaidizi mpya, Abdulhamid Moalin, ambaye amejiunga na benchi la ufundi kwa lengo la kushirikiana na kocha mkuu Pedro Goncalves kuimarisha zaidi kikosi hicho.
Yanga inatarajiwa kuingia kambini kuanzia kesho kuanza maandalizi rasmi ya michezo ya duru la pili, wakianzia na pambano dhidi ya Tanzania Prisons litakalochezwa Aprili 4 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa kujiamini, Kamwe amesema kikosi hicho kimejipanga kuhakikisha hakipotezi alama yoyote katika mzunguko wa pili, akisisitiza kuwa ushindani uliopo hautawatisha.
“Kama kuna timu haijapata sare katika duru la kwanza basi imekula kwao. Sisi tumejipanga vizuri na katika mzunguko wa pili hatutapoteza pointi, tutakuwa imara zaidi,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa tayari Moalin amewasili nchini na kufanya vikao na benchi la ufundi chini ya Goncalves, jambo linaloashiria kuwa maandalizi yote yanaenda kama yalivyopangwa kuelekea hatua hiyo muhimu ya ligi.
Kwa mujibu wa Kamwe, maboresho yaliyofanywa na mipango waliyojiwekea vinawapa uhakika wa kumaliza msimu wakiwa katika kiwango cha juu bila kuyumba.
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 baada ya kucheza mechi 16, huku Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 31 baada ya mechi 14 na kiporo cha michezo miwili.
Macho na masikio ya wengi yataelekezwa kwenye dabi ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba katika duru la pili, mchezo unaotarajiwa kuwa na uzito mkubwa katika kuamua hatima ya ubingwa wa msimu huu.