Home Habari za michezo SIMBA WAREJEA NA MIPANGO MADHUBUTI KUMDHIBITI MPINZANI

SIMBA WAREJEA NA MIPANGO MADHUBUTI KUMDHIBITI MPINZANI

0

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewahakikishia mashabiki kuwa kikosi cha timu hiyo kipo tayari kurejea dimbani kwa nguvu kubwa baada ya mapumziko mafupi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ahmed amesema kuwa zimesalia siku chache tu kabla ya Simba kurejea kwenye michuano ya ligi, ambapo Aprili 2 watashuka dimbani kuikabili Coastal Union katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Amesisitiza kuwa kikosi hicho kinahitaji kujiandaa kikamilifu, akiongeza kuwa mpambano huo hautakuwa mwepesi kwani wapinzani wao wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri. Lazima Simba wajipange kwa umakini ili kufanikisha malengo yao ya ushindi.

“Mashabiki wa Simba, tujitokeze kwa wingi uwanjani siku hiyo ili kuwapa morali wachezaji wetu. Sapoti yao imekuwa chachu muhimu ya mafanikio ya timu katika michezo mbalimbali,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa uwepo wa mashabiki uwanjani umekuwa ukibadilisha kabisa taswira ya mchezo, akirejelea mfano wa mechi iliyopita dhidi ya TRA United, ambapo sapoti kubwa ilichangia timu kupata matokeo chanya.

Simba inaonekana kuwa na hamasa kubwa kuelekea mchezo huo muhimu, huku benchi la ufundi likiendelea kuwanoa wachezaji kuhakikisha wanakuwa katika ubora wa hali ya juu wanaporejea dimbani.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa Simba katika harakati zao za kusaka ubingwa, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona timu yao ikirejea kwa kishindo kwenye ushindani wa ligi.