Home Habari za michezo YANGA WATESEKA WANAWAKE, SIMBA WAZIDI KUTIKISA LIGI

YANGA WATESEKA WANAWAKE, SIMBA WAZIDI KUTIKISA LIGI

0

Wakati katika Ligi Kuu Tanzania Bara ya wanaume Yanga ikiendelea kuongoza msimamo, hali ni tofauti kabisa upande wa wanawake ambapo Simba Queens ndiyo wanaoshika usukani wa ligi hiyo.

Kwa upande wa wanaume, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 44 huku Simba ikifuatia na pointi 35, ikiwa nyuma kwa michezo miwili kabla ya kukutana na TRA United katika mchezo wa jioni ya leo.

Hata hivyo, kwenye Ligi ya Wanawake, Simba Queens wameendelea kuonyesha ubora wao na kuongoza msimamo, huku mbio za ubingwa zikichukua sura mpya baada ya Yanga Princess kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa 13. Yanga Princess walichapwa mabao 2-0 na Tausi Women katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Matokeo hayo yameifanya Yanga Princess kubaki nyuma ya vinara Simba Queens, ambao sasa wameongeza pengo la pointi hadi nne baada ya kufikisha pointi 37 kufuatia ushindi walioupata dhidi ya Bunda Queens ugenini kwenye Uwanja wa Karume mkoani Mara.

Kabla ya michezo hiyo, Yanga Princess walikuwa nyuma kwa pointi moja tu, lakini kupoteza huko kumewaweka kwenye presha kubwa ya mbio za ubingwa, hasa ikizingatiwa kuwa bado hawajawahi kutwaa taji la ligi hiyo.

Kwa upande wa Tausi Women, ushindi huo umeipa timu hiyo morali mpya baada ya kufikisha pointi 15 na kupanda hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.

Katika michezo mingine, Ceasiaa Queens ililazimishwa sare tasa na Alliance Girls katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa, huku Mashujaa Queens ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruangwa Queens kwenye Uwanja wa Kituo cha TFF Kigamboni.

Sasa Yanga Princess wanalazimika kushinda michezo yao ijayo bila makosa ili kuendelea kubaki kwenye mbio za ubingwa. Wakati huo huo, wanahitaji matokeo mabaya kutoka kwa Simba Queens, jambo linaloonekana kuwa gumu kutokana na kiwango kizuri wanachoonyesha vinara hao wa ligi.