Habari za michezo
SOWAH NJIANI KUTOKA, SIMBA KUWINDA MBADALA WAKE
Vardo
April 11, 2026
2:26 pm
UONGOZI wa klabu ya Simba umeeleza kuwa tayari umeanza mikakati ya kuingia sokoni kwa ajili ya usajili wa dirisha kubwa lijalo, huku ukithibitisha kuwa mazungumzo na baadhi ya wachezaji yameanza rasmi.
Imebainishwa kuwa miongoni mwa maeneo wanayoyapa kipaumbele ni kusaka mshambuliaji mpya atakayechukua nafasi ya Jonathan Sowah, ambaye inaelezwa hana mustakabali ndani ya kikosi hicho.
Akizungumza kuhusu mchakato huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo inalenga kupata mshambuliaji hatari atakayesaidia kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji kuelekea michezo ijayo.
“Tupo sokoni kwa sasa tukitafuta mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao. Usajili ni mchakato unaoendelea hata wakati ligi inaendelea.
Mara nyingi klabu hufanya makosa kwa kusubiri hadi dirisha lifunguliwe rasmi ndipo waanze harakati, jambo ambalo hata sisi tulishawahi kukumbana nalo,” amesema Ahmed.
Amefafanua kuwa kuchelewa kuanza usajili kunaweza kusababisha klabu kutumia fedha nyingi zaidi kumsajili mchezaji kuliko thamani yake halisi, kutokana na ushindani na uharaka wa kufanya maamuzi.
“Unakuta mchezaji ambaye angepatikana kwa gharama ndogo, analetwa kwa bei kubwa kwa sababu ya kuchelewa kufanya maamuzi sahihi. Ili kuepuka hilo, sisi tumeanza mapema,” ameongeza.
Ahmed amesisitiza kuwa Simba inafuata utaratibu wa kitaaluma katika usajili, kwa kuhakikisha kwanza wanapitia mikataba ya wachezaji kabla ya kuanza mazungumzo.
“Kama tumemvutiwa na mchezaji, kwanza tunaangalia mkataba wake unasemaje. Kama unaruhusu kuzungumza naye moja kwa moja, tunafanya hivyo. Kama hauwaruhusu, basi tunafuata taratibu za kuwasiliana na klabu husika,” amesema.
Ahmed amesema lengo la Simba ni kuhakikisha kipindi cha usajili kinakuwa cha kutangaza tu wachezaji waliokwishakamilisha taratibu zote, badala ya kuanza harakati za dharura ambazo mara nyingi husababisha kufanya maamuzi yasiyo sahihi.