UONGOZI wa Simba SC umefikia uamuzi wa kuachana na kipa wake Moussa Camara mwishoni mwa msimu huu, baada ya mkataba wake kufikia tamati.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mkataba wa Camara unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, na tayari uongozi umeshamjulisha kupitia upande wake wa usimamizi kuwa hautaongeza mkataba mpya.
Camara, ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha, ameshuhudia nafasi yake ikichukuliwa na ujio wa kipa Mahamadou Kassali, ambaye ameonyesha kiwango kizuri na kujiimarisha kama chaguo la kwanza golini.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Kassali ameweza kujiamini na kutoa matokeo bora, hali iliyowafanya mabosi wa Simba SC kuanza kupanga mustakabali wa safu yao ya makipa bila kumhusisha Camara kwa msimu ujao.
“Camara hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu ujao, huku Kassali akiendelea kubaki kutokana na kiwango chake kizuri,” ameeleza mtoa taarifa wa ndani ya klabu.
Kwa sasa, Simba SC inaendelea kuwategemea makipa wake wawili waliobaki ambao ni Kassali na Hussein Abel, huku Yakubu Suleiman naye akiendelea na mapambano ya kuuguza majeraha yake.