NAHODHA wa Simba, Shomari Kapombe, amesisitiza umuhimu wa timu yake kuhakikisha inapata ushindi katika kila mechi wanayocheza, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza pengo la pointi dhidi ya wapinzani wao wakubwa, Yanga, kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kapombe amesema ushindani wa ligi hiyo msimu huu umeongezeka kwa kiasi kikubwa, hali inayowalazimu wachezaji wa Simba kuongeza juhudi na umakini ili kufanikisha malengo yao.
Ameeleza kuwa hakuna nafasi ya kufanya makosa, kwani kila alama ina mchango mkubwa katika msimamo wa ligi.
Kwa sasa, Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 17, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi. Tofauti ya pointi nane dhidi ya Yanga wanaoongoza kwa pointi 44 baada ya mechi 18, imekuwa kichocheo kikubwa kwa Simba kuongeza kasi ya ushindani.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Kapombe amesema kuwa kikosi chao kimejipanga vyema kuhakikisha kinapambana hadi mwisho wa msimu.
Amesema wanachukulia kila mchezo kwa uzito mkubwa kana kwamba ni wa fainali, ili kuongeza nafasi ya kushinda na kuendelea kukusanya alama tatu muhimu.
“Tunapambana kupunguza pengo la pointi dhidi ya Yanga katika mbio za ubingwa. Kwetu sisi kila mechi ni kama fainali. Hatutadharau timu yoyote, tunaiheshimu kila mpinzani na kuuchukulia kwa uzito unaostahili,” amesema Kapombe.
Nahodha huyo ameongeza kuwa morali ya wachezaji ndani ya kikosi hicho ipo juu, na kila mmoja anaelewa wajibu wake katika kuhakikisha timu inafanya vizuri.
Ameeleza kuwa ushirikiano, nidhamu na kujituma ndio silaha kuu wanazozitegemea katika kipindi hiki muhimu cha msimu.
Pamoja na changamoto zilizopo, Kapombe ameonesha matumaini makubwa kuwa Simba ina uwezo wa kufikia malengo yake, akisisitiza kuwa ligi bado ina michezo mingi na chochote kinaweza kutokea.
Amesema kwa kuwataka mashabiki kuendelea kuwaunga mkono, kwani mchango wao ni muhimu katika safari ya kusaka ubingwa.