Home Habari za michezo VITA YA MABEKI SIMBA DHIDI YA MASHINE YA MABAO NGOY

VITA YA MABEKI SIMBA DHIDI YA MASHINE YA MABAO NGOY

0

BEKI wa Simba SC wanakabiliwa na mtihani mzito wa kuhakikisha wanamdhibiti mshambuliaji hatari wa Namungo FC, Fabrice Ngoy, ili kuzuia hatari ya kutikisa nyavu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Kikosi cha Simba kimeanza safari kuelekea Ruangwa kwa ajili ya mchezo huo muhimu, ambapo kitakuwa ugenini kuikabili Namungo FC Aprili 19 katika Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi.

Safu ya ulinzi ya Simba, inayoongozwa na Shomari Kapombe, Rushine De Reuck pamoja na Toure, inatarajiwa kuwa imara kuhakikisha inamzuia Ngoy ambaye amekuwa katika kiwango bora na kinara wa mabao kwa upande wa Namungo.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi kipo tayari kwa mchezo huo licha ya ratiba kuwa ngumu.

Ameeleza kuwa baada ya kurejea Dar es Salaam kutoka Arusha, timu imepata muda wa kujipanga upya kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ruangwa kwa ajili ya pambano hilo muhimu.

“Kila mechi iliyobaki ni ya ushindani mkubwa, hatuna nafasi ya kuidharau timu yoyote. Tunakwenda kukutana na timu nzuri yenye safu imara ya ushambuliaji,” amesema Ahmed.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na presha ya kusaka ushindi ili kuendelea kupunguza pengo la alama dhidi ya vinara wa ligi, hali inayoongeza uzito na mvuto wa pambano hilo.