HATUA ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB imepangwa rasmi kuchezwa Mei16 hadi 17 , huku vigogo wa soka Tanzania wakitarajiwa kushuka dimbani kusaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali katika michuano hiyo yenye ushindani mkubwa.
Katika ratiba hiyo, Simba SC watakuwa na kibarua kizito watakapokutana na TRA United, mchezo unaotarajiwa kuwa na presha kubwa kutokana na kila timu kuhitaji ushindi ili kusonga mbele. Simba wataingia wakiwa na uzoefu mkubwa wa michuano, lakini TRA United nao hawapaswi kubezwa.
Kwa upande mwingine, JKT Tanzania watamenyana na mabingwa watetezi Yanga SC katika pambano linalotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi. Yanga wataingia na rekodi nzuri ya ushindi, huku JKT Tanzania wakisaka kufanya mapinduzi na kuiondoa njiani timu hiyo kubwa.
Mashujaa FC wao watakutana na Azam FC katika mchezo mwingine wa robo fainali utakaokuwa na ushindani mkali. Azam wanaonekana kuwa na kikosi imara, lakini Mashujaa FC nao wameonyesha uwezo wa kushindana na timu kubwa katika msimu huu.
Katika mechi nyingine, Coastal Union watapambana na Singida Black Stars, huku kila timu ikiwa na ndoto ya kufika mbali zaidi katika mashindano hayo. Huu ni mchezo ambao unaweza kuamua kwa makosa madogo kutokana na ubora wa timu zote mbili.
Kwa mujibu wa upangaji wa ratiba hiyo, mshindi kati ya Simba SC na TRA United atakutana na mshindi wa mchezo kati ya Coastal Union na Singida Black Stars katika hatua ya nusu fainali, hali inayoweza kuleta pambano kali la kuwania tiketi ya fainali.
Aidha, mshindi wa mechi kati ya JKT Tanzania na Yanga SC atachuana na mshindi wa pambano la Mashujaa FC dhidi ya Azam FC katika nusu fainali, hatua inayotarajiwa kuwa na mvutano mkubwa kuelekea fainali ya michuano hiyo.