SIMBA imeshinda mchezo wa pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara ikiwa ugenini baada ya kuichapa Namungo mabao 3-0, ikizidi kuweka hai kiu yao ya kuutaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na sasa kituo kinachofuata ni pale itakaporudi nyumbani kuwakaribisha Yanga inayoongoza ligi.
Ikitoka kuichapa Fountain Gate 3-0, leo Aprili 19, 2026 ilikuwa zamu ya Namungo ambapo timu hizo mbili msimu huu ndio zilizoruhusu mabao sita kila moja kwenye mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Simba.
Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikishinda mchezo wa 12 kati ya 19 iliyocheza, ikifikisha pointi 42, tano nyuma ya Yanga yenye 47.
Alikuwa Elie Mpanzu tena akitokea benchi na kuihakikishia Simba ushindi kwa bao lake la tatu lililoifanya timu hiyo kushusha presha, ikiwa ni mechi ya pili kwa Mkongomani huyo kufanya hivyo kama alivyotangulia dhidi ya Singida Black Stars.
Simba ushindi wake huo ulitokana na mabao ya mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa mawinga, Libase Gueye aliyefunga dakika ya 11 akimalizia pasi ya beki Antony Mligo, Msenegali huyo akiendeleza kasi ya kufunga akifikisha bao la nne msimu huu.
Bao la pili kwa wekundu hao likapatikana dakika ya 25, likifungwa na winga Anicet Oura kwa shuti la nje ya eneo la hatari, likiwa pia ni bao lake la tatu msimu huu katika ligi, huku Namungo bao lao likifungwa dakika ya 34 na Heritier Makambo kwa njia ya mkwaju wa penalti iliyotokana na kiungo wa Simba, Yusuph Kagoma kushika mpira kwenye eneo la hatari. Mpaka mapumziko timu hizo zilienda mapumziko huku wageni wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Mabadiliko mawili ya mapema kipindi cha pili kwa Simba akitolewa mshambuliaji Seleman Mwalimu akiingia Mpanzu na pia kutolewa Inno Loemba nafasi yake ikienda kwa Neo Maema dakika ya 63, ndio yalikuja kuwabeba Wekundu hao wa Msimbazi kwa Mpanzu kupiga bao la tatu kwenye mchezo huo, lakini pia likiwa la tatu kwake kwenye ligi.
TATU YA SITA
Simba bado inasubiri kuona ni lini itashinda mabao manne msimu huu ambapo mpaka sasa ushindi wake mkubwa ni mabao matatu, ilizozipiga Fountain Gate na Namungo mara mbili zikipoteza nyumbani na ugenini, TRA United na Mbeya City.
MAKAMBO BAO LA KWANZA
Makambo ambaye aliifungia bao pekee la Namungo, hilo linakuwa la kwanza kwake msimu huu akiwa amekumbana na ukame mkubwa wa kufunga akisotea benchi kwenye mechi nyingi lakini pia linakuwa bao la kwanza kuifunga Simba tangu atue nchini akitokea kwao DR Congo.
Baada ya mchezo huo, Simba itasafiri kwenda Zanzibar kuanza mashindano ya Kombe la Muungano lakini pia tetesi zikienea kwamba mchezo wake unaofuata wa ligi kuna uwezekano wa kuchezwa kisiwani humo dhidi ya Yanga, Mei 3,2026.