LEO Uwanja wa Majaliwa unatarajiwa kuwa kitovu cha burudani na ushindani mkali, pale Namungo FC watakapowakaribisha Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaobeba hisia na presha kubwa kwa pande zote mbili.
Mchezo huu unakutanisha mitindo tofauti ya soka, huku kila timu ikiwa na kiu ya kupata matokeo chanya. Uzito wake unaongezeka kutokana na hadhi ya ligi hiyo, ambayo ni miongoni mwa ligi sita bora barani Afrika, hali inayoongeza ushindani na kiwango cha mchezo.
Ndani ya dimba, macho mengi yatakuwa kwenye safu za ulinzi za timu zote mbili. Mabeki wanatarajiwa kuwa na kazi kubwa ya kuwadhibiti washambuliaji hatari watakaokuwa na jukumu la kuamua matokeo ya mchezo huo.
Kwa upande wa Simba SC, safu ya ulinzi ikiongozwa na Rushine De Reuck, David Kamenta, Ismael Olivier Toure pamoja na Nickson Kibabage, italazimika kuwa makini zaidi kumkabili mshambuliaji kinara wa Namungo FC, Fabrice Ngoy, ambaye amekuwa tishio mbele ya lango.
Kocha Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kwa mtihani huo mgumu. Amesema maandalizi yamekamilika vizuri na wachezaji wako katika hali nzuri ya kupambana, akisisitiza kuwa kucheza nyumbani ni faida kwao huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao.
Kwa upande wa Simba SC, Kocha Mkuu Steve Barker ameonyesha tahadhari kubwa kuelekea mchezo huo, akitambua ubora wa wapinzani wao. Amesisitiza umuhimu wa nidhamu ya hali ya juu kwa wachezaji wake ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini.
Katika msimamo wa ligi, Simba SC wanashika nafasi ya pili wakisaka kuendelea kubaki kwenye mbio za ubingwa, huku Namungo FC wakiwa nafasi ya kumi wakipambana kuboresha nafasi yao. Tofauti hii ya malengo inaongeza uzito wa mchezo huo.
Upande wa ushambuliaji nao utavutia macho ya wengi, ambapo Fabrice Ngoy wa Namungo FC anaongoza kwa mabao nane, huku Simba SC wakimtegemea Seleman Mwalimu ambaye tayari ameshafunga mabao sita msimu huu.
Kwa ujumla, mchezo wa leo una kila sifa ya kuwa pambano la kiwango cha juu, ambapo nidhamu ya mchezo, mbinu za makocha na ubora wa wachezaji vitachukua nafasi kubwa katika kuamua nani ataondoka na pointi tatu muhimu kutoka Uwanja wa Majaliwa.