UONGOZI wa klabu ya Yanga umeibua mjadala mpya kwenye soko la usajili baada ya kuelezwa kuwa umeanza kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Wydad AC ya Morocco, Selemani Mwalimu, ambaye kwa sasa anaitumikia Simba kwa mkopo.
Mwalimu ambaye amejiunga na Simba kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita, ameonyesha kiwango bora na kuvutia macho ya wadau mbalimbali wa soka kutokana na uwezo wake wa kufunga na mchango wake uwanjani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoaminika, mshambuliaji huyo anatarajiwa kurejea Wydad AC mwishoni mwa msimu huu baada ya kumaliza muda wake wa mkopo ndani ya kikosi cha Simba SC, ambacho kimekuwa kikinufaika na ubora wake.
Inaelezwa kuwa mafanikio yake akiwa Simba yamezifanya baadhi ya klabu kubwa, ikiwemo Yanga, kuanza kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wake kwa lengo la kumshawishi kabla ya kurejea Morocco.
Chanzo cha ndani kimeeleza kuwa Yanga chini ya uongozi wa Rais Hersi Said wameanza mawasiliano ya awali na upande wa mchezaji huyo kupitia klabu yake ya Wydad AC ili kujua uwezekano wa kumpata.
“Kwa sasa Mwalimu ni miongoni mwa washambuliaji wazawa wanaofanya vizuri zaidi. Viongozi wameanza kufuatilia mkataba wake Wydad AC kuona kama kuna nafasi ya kumpata au la,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, bado haijafahamika kama Wydad AC wako tayari kumruhusu mchezaji huyo kuondoka kirahisi, huku vita ya usajili kati ya vigogo wa soka la Tanzania ikiendelea kuchukua sura mpya.