BONDIA wa kimataifa wa ngumi za kulipwa nchini, Ibrahimu Class, ameandika historia mpya baada ya kupata ushindi wa kishindo dhidi ya mpinzani wake Kritiphak Duangnut kwa TKO katika raundi ya tano, kwenye pambano lililopigwa jijini Bangkok, Thailand, usiku wa kuamkia leo.
Katika pambano hilo, Class alianza kwa tahadhari kubwa ndani ya raundi mbili za mwanzo, akionekana kusoma mbinu na mwenendo wa mpinzani wake kabla ya kuachia makonde yake mazito.
Kuanzia raundi ya tatu, alibadilika kabisa na kuanza kulitawala pambano hilo kwa kuonyesha kasi, nguvu na umakini wa hali ya juu.
Mashambulizi yake makali yaliendelea kumuweka Duangnut kwenye presha kubwa, hali iliyomfanya kushindwa kuhimili makonde ya Class. Kadri raundi zilivyokuwa zikisonga mbele, ilikuwa wazi nani alikuwa akiongoza pambano hilo.
Kabla ya refa kusimamisha pambano katika raundi ya tano, Duangnut tayari alikuwa ameangushwa chini mara tatu, ishara tosha ya ubora na uthabiti wa Class katika usiku huo wa ushindi.
Ushindi huo unamfanya Ibrahimu Class kutwaa ubingwa mpya wa kimataifa wa WBC katika uzani wa kilo 59, huku pia akifanikiwa kulipiza kisasi baada ya pambano lao la awali kuisha kwa sare miezi kadhaa iliyopita.